YUPI MZAZI NA MTOTO KATI YA SERIKALI NA WANANCHI?


Japo miaka mingi imepita tukiwa tunasubiri kuwa labda kesho ikifika tutakuwa na japo unafuu, na hali huwa tofauti, basi ni bora sasa kwa kila mwenye nguvu, akili na utashi ajitokeze aingie uwanjani kutetea jamii yake.
Tunaona kilasiku vyombo vya habari vikitoa lawama kwa serikali na viongozi wake. Pengine ni halali kwa lawama hizo, japo kwa upande mwingine tutakuwa tunawakosea viongozi na serikalizetu, na hili limeletwa na sisi wenyewe, hatuna budi kuwaacha wafanye wanavyotaka kwani tumewajengea msingi wa kuwa hivyo.
Hebu tujiulize kuwa, mwenye jukumu la kumlea mtoto katika familia ni nani? Bila shaka jibu ni kuwa, baba na mama ndio wahusika wakuu, na ni nani wa kwanza kupewa lawama endapo mtoto ameharibikiwa, ana tabia isiyofaa kuigwa? Ni wazazi au mtoto mwenyewe? Kama jibu ni mzazi, iweje leo tumegeuka na kumlaumu dobi kutotakasa kaniki hali rangi yake twaijua? Sisi na viongozi serikalini nani ni mzazi kwa mwenzake?... Kwa mtazamo wa wengi ni kuwa viongozi serikalini ndio wazazi halafu wananchi ndio watoto, lakini kiuhalisia, wananchi ndio wazazi na viongozi serikalini ni watoto wa wananchi.
Kwani hao viongozi waliwekwa na nani katika vyeo hivyo? Bila shaka ni wananchi ambao kwao ndio uzao wao kupitia chaguzi mbalimbali ikazaliwa serikali na viongozi. Iweje leo baba amekuwa mwana na mwana akawa baba?
Inasikitisha kuona kuwa wananchi tumeshindwa kuilea serikali yetu ikawa ya manufaa, badala yake tumebaki kulaumu. Hebu jiulize, ni mara ngapi ulimtafuta kiongozi wako ukajadiliana naye kuhusu namna anavyo endesha uongozi wake? Au ni mara ngapi umemuelekeza mbinu bora za uongozi? Au tunaloweza ni kukaa na kulaumu kuwa kiongozi yule hafai. Wewe ukiwa kama mzazi uliyemtuma mwanao akafanye kazi matokeo yake akaharibu umechukua hatua gani?....
Hawa ni watoto wetu tena tulio wazaa kwa uchungu pengine hata damu zilitutoka, leo wametugeuza watoto wa mtaani tusiojua kesho yetu, na sisi bila aibu tupo majaani tukichakura mabaki waliyotupa.
Lahasha, hii sio halali na wala sio utamaduni wetu, yatupasa turudie mila zetu, tukae na wanetu, tuwafundishe namna ya kuishi na kuheshimu wengine, tusiishie kusema "asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu" huu ni uvivu wa kutotaka kuwajibika, na tusiusingizie utandawazi, chanzo cha tatizo ni sisi na suluhisho ni sisi wenyewe, katika mila zetu, kama mtu akionywa hasikii basi hutengwa na wenzake, hivyo kama hawa watoto tulio wazaa leo hawatusikilizi, hatunabudi kuwaondoa katika familia zetu, waende huko watakapowapata wazazi wanaopenda watoto watukutu.
Tukiamua tunaweza, sisi sio masikini bali watoto tuliowazaa tukawapa mamlaka hadi ya kutugandamiza ndio wanaotufa masikini, wanatuibia nasi tunamwachia Mungu, Hivi Mungu afanye mangapi?!
Nina kila sababu ya kutosubiri kesho, maana watoto sahivi wajanja, ikifika keshe ya jana wanakuambia kesho ya leo, kwani kesho ya jana iko wapi? Na leo ya kesho iko wapi?.... Kwa mtindo huu tutangoja hadi mwisho wa nyakati.

Ni mtazamo usio na maana kwa hao tunaowaita baba ilihali ni watoto, bali kwetusisi watoto baba inafaa tuzingatie.

No comments

Thank for your coment

Powered by Blogger.