Waziri wa nishati na madini Willium Ngeleja amtetea Raisi Kikwete

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amesema tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu uundwaji wa Katiba mpya itakuwa huru na haitaingiliwa na mamlaka yoyote na kwamba hata Rais Jakaya Kikwete hatakuwa na mamlaka ya kuingilia kazi ya tume licha ya kuiunda.
Akizungumza kwenye mkutano maalumu wa CCM ulioandaliwa kwa ajili ya kuwapokea wanachama wapya 30 kutoka CHADEMA mjini hapa juzi, Ngeleja alisema upotoshwaji unaoenezwa na baadhi ya wanasiasa nchini kwamba tume hiyo haitakuwa huru kwa kuwa itaundwa na Rais anayetokana na CCM si kweli na aliwaonya wanasiasa hao kuacha mara moja hulka hiyo.


Ngeleja alisema tume hiyo itafanya kazi zake kwa kufuata taratibu na sheria za nchi na si matakwa ya mtu au kiongozi yeyote na kwamba itakusanya maoni ya wananchi kwa miezi 18, hivyo Watanzania wanapaswa kupuuza upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya wanasiasa.
“Naomba niwahakikishie Watanzania kwamba tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya itakayoundwa na Rais itakuwa huru na haitaingiliwa na mtu yeyote. Hata Rais hawezi kuingilia kazi ya tume.
“Wapo watu wanawapotosha Watanzania eti tume haitakuwa huru kwa kuwa imeundwa na Rais anayetokana na CCM. Kwa kweli mawazo yao siyo sashihi,” alisema Ngeleja.
Hata hivyo, Ngeleja  aliwashangaa wanasiasa na watu wengine wanaopiga kelele kuhusu sheria ya mabadiliko ya Katiba mpya ya mwaka 2011, iliyopitishwa Bungeni na kusainiwa na Rais Kikwete, na kusema sheria hiyo imetungwa na kupitishwa kama zinavyopitishwa sheria nyingine.
Alisema Rais Kikwete alichosaini siyo Katiba mpya, bali ni sheria ya namna ya mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya utakavyokuwa na kwamba hata Bunge halijapitisha Katiba mpya na aliwaomba watu kama hawaujui mchakato huo ni bora wakanyamaza, maana wakiendelea kuupotosha umma mtu huyo anaweza kueleweka hana akili sawasawa.
Kwa mujibu wa Ngeleja, Rais anatarajiwa kuunda Bunge la Katiba kwa kuwashirikisha wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wawakilishi wa Baraza la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), na wajumbe wengine 166 kutoka asasi mbalimbali za kiraia.
Alizitaja baadhi ya asasi hizo zitakazoshiriki kwenye Bunge la Katiba kuwa ni madhehebu ya dini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu, makundi maalumu ya kijamii, vyama vya wafanyakazi, jumuiya ya wakulima, wafugaji, vikundi vingine vya watu vyenye malengo yanayofanana.

No comments

Thank for your coment

Powered by Blogger.